Sunday, July 31, 2011

NYAKATI 3 MUHIMU ZA KUFANYA IBADA KATIKA MWEZI MTUKUFU WA RAMADHAN


Nyakati Tatu Muhimu Za Kufanya Ibada – Zisikupite Katika Ramadhaan
 
Nyakati tatu hizi ni muhimu sana za kufanya ibada kutokana na fadhila zake kuu. Mwenye kupenda kuchuma thawabu nyingi asizikose khaswa katika mwezi huu Mtukufu Wa Ramadhaan ambao ni mwezi wenye malipo maradufu
1-Wakati wa mwanzo:  Baina ya Alfajiri na jua kuchomoza:
Usimulizi uliothibiti kutoka katika Swahiyh Muslim (564/1) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba walikuwa wakibakia macho wakati huo hadi jua kuchomoza kwani ni wakati mja anapogaiwa rizki yake, na ni wakati wenye kheri nyingi, unampa siha nzuri ya mwili binaadamu, na kwa ujumla ni wakati wenye baraka nyingi za kila aina kwani Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliomba: 
((اللهم بارك لأمتي في بكورها))  الترمذي, أحمد, أبي داود, ابن ماجه 
((Ewe Allaah, wabarikie Ummah wangu nyakati za asubuhi mapema)) [At-Tirmidhiy, Ahmad, Abu Daawuud, Ibn Maajah na imethibitishwa kuwa ni Hadiyth Swahiyh na Shaykh Al-Albaaniy]
Usimulizi huu umetoka kwa Maswahaba kadhaa ambao wameelezea kwamba: "Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipotaka kupeleka kikosi au jeshi aliwapeleka mwanzo wa asubuhi". Vile vile wamesimulia kwamba: "Swakhar alikuwa mtu tajiri ambaye alikuwa akipelekea biashara zake mwanzo wa asubuhi na matokeo yake ilikuwa ni kufuzu katika biashara na kupata faida kubwa sana".
Wamesimulia Salafus-Swaalih kwamba Ibn 'Abbaas naye alimkataza mtu kulala nyakati hizo alipomwambia: 
   "قُم، أتنام في الساعة التي تقسَّم فيه الأرزاق؟"
"Inuka! Je, unalala katika saa ambayo rizki inagaiwa?"
Ikiwa basi wakati huo ni kama hivyo ilivyoelezwa juu, basi vipi Muislamu auache wakati huu umpite khaswa katika mwezi huu mtukufu wa Ramdhaan?
Ibnul-Qayyim (Rahimahu-Allaah) katika kitabu chake 'Zaad Al-Ma'aad' amesema: "Usingizi wa asubuhi unanyima rizki kwani huo ni wakati ambao Muumba anaombwa rizki na wakati wa kugaiwa rizki. Hivyo usingizi unanyima rizki isipokuwa kwa dharura. Usingizi wakati huo pia ni madhara kwa mwili…"  

Faida nyingine kubwa ya kubakia macho ukimdhukuru Allaah wakati huu:  
Si chini ya muda wa saa na nusu utakuwa umepata thawabu za Hajj na ‘Umrah kamilifu:
عن أنس عن النبي صلى الله عليه وسلم ، أنه قال  (( من صلى الفجر في جماعة ثم قعد يذكر الله  حتى تطلع الشمس ثم صلى ركعتين كانت له كأجر حجة وعمرة تامة تامة تامة) ) أخرج الترمذي  صححه الألباني .
Imetoka kwa Anas kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayeswali Alfajiri katika Jama'ah kisha akakaa anamkumbuka Allaah mpaka likachomoza jua kisha akaswali Raka'ah mbili, atapata ujira kama ujira wa kwenda Hajj na 'Umrah ulio kamili kamili kamili)) [Imetolewa na At-Tirmidhiy na kaisahihisha Al-Albaaniy]
Pindi ukifanya hivyo kwa mwezi mzima utakuwa umechuma thawabu za Hajj na ‘Umrah mwezi mzima. Hizo ni fadhila za siku za kawaida, seuze ukifanya mwezi mtukufu huu wa Ramadhaan? Jitahidi ndugu Muislamu kadiri uwezavyo kuchuma hizi thawabu kubwa ambazo zingelikukalifu mali, tabu za safari na mashaka ya kufika Makkah kutekeleza ibada hizo. Lakini kwa Rahma ya Allaah Ametujaalia tuweze kuzichuma tukiwa majumbani mwetu tena kwa wepesi kabisa. Wanaume thawabu zitazidi ikiwa watatekeleza wakiwa misikitini. Wanawake wanazipata fadhila hizo hata wakiswali majumbani mwao.  Hata hivyo, pamoja na ujira wote huu, tusisahau kuwa fadhila hizo hazivunji wala hazifuti fardh ya kwenda Hajj kwa mwenye uwezo, asije mtu akadhani kufanya hayo kutakuwa kumetengua wajiibu wake wa kuhiji au kufanya ‘Umrah.
2- Wakati wa pili: Kabla ya Jua kuzama (Magharibi):
Huu ni wakati ambao bado Muislamu yuko katika Swawm na du'aa yake anayoiomba hairudi:
 قال صلى الله عليه وسلم: ((ثلاثة لا ترد دعوتهم: الصائم حتى يفطر والإمام العادل والمظلوم))  وروى الترمذي   بسند حسن
Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: (([Watu] watatu du'aa zao hazirudi; mwenye kufunga hadi afuturu/afutari, Kiongozi muadilifu na aliyedhulumiwa)) [At-Tirmidhiy kwa isnaad nzuri]
Kwa hiyo ni fursa ya kuitumia Muislamu aombe du'aa na haja zake wakati huu khaswa pia kwa vile ni wakati ambao Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amehimiza Atukuzwe kama Anavyosema:
 (( وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ قَبْلَ طُلُوعِ الشَّمْسِ وَقَبْلَ الْغُرُوبِ))   
((.. na mtakase kwa kumsifu Mola wako Mlezi kabla ya kuchomoza jua na kabla ya kuchwa)) [Qaaf: 39]
  
 ((وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ قَبْلَ طُلُوعِ الشَّمْسِ وَقَبْلَ غُرُوبِهَا وَمِنْ آنَاء اللَّيْلِ فَسَبِّحْ وَأَطْرَافَ النَّهَارِ لَعَلَّكَ تَرْضَى)) 
((…Na umtakase Mola wako Mlezi kwa kumsifu kabla ya kuchomoza jua, na kabla halijachwa, na nyakati za usiku pia umtakase, na ncha za mchana ili upate ya kukuridhisha)) [Twaahaa: 130]. 
 (( وَاسْتَغْفِرْ لِذَنبِكَ وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ بِالْعَشِيِّ وَالْإِبْكَار)) 
((…Na omba msamaha kwa dhambi zako, na umtakase Mola wako Mlezi kwa kumhimidi jioni na asubuhi)) [Ghaafir: 55]   
3- Wakati wa tatu: Suhuur - Kabla ya Alfajiri
Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amewaaahidi Wacha Mungu Pepo kwa sababu sifa mojawapo yao ni kuomba maghfira kabla ya Alfajiri: 
 إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي جَنَّاتٍ وَعُيُون)) ((آخِذِينَ مَا آتَاهُمْ رَبُّهُمْ إِنَّهُمْ كَانُوا قَبْلَ ذَلِكَ مُحْسِنِينَ))  ((كَانُوا قَلِيلًا مِّنَ اللَّيْلِ مَا يَهْجَعُونَ))  ((وَبِالْأَسْحَارِ هُمْ يَسْتَغْفِرُون))

((Hakika Wacha Mungu watakuwa katika Mabustani na chemchem)) ((Wanapokea Aliyowapa Mola wao Mlezi. Kwa hakika hao walikuwa kabla ya haya wakifanya mema)) ((Walikuwa wakilala kidogo tu usiku)) ((Na kabla ya Alfajiri wakiomba maghfira)) [Adh-Dhaariyaat: 15-18]

  
Kisha wamesifiwa tena kwa sifa hiyo hiyo pamoja na nyinginezo:
((الصَّابِرِينَ وَالصَّادِقِينَ وَالْقَانِتِينَ وَالْمُنفِقِينَ وَالْمُسْتَغْفِرِينَ بِالأَسْحَارِ))   
((Wanaosubiri, wanaosema kweli, na watiifu, na wanaotoa sadaka, na wanaoomba maghafira kabla ya Alfajiri)) [Al-'Imraan: 17]
Muislamu asiache wakati huo umpite kwani ni wakati muhimu na wenye fadhila na faida kubwa kwa vile Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Huteremka wakati huo kutoka mbingu ya saba na kuweko mbingu ya ardhi kutukidhia haja zetu:
 عن أبي هريرة رضي الله عنه أن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال: ((ينزل ربنا تبارك وتعالى كل ليلة إلى السماء الدنيا حين يبقى ثلث الليل الآخر فيقول: من يدعوني فأستجيب له؟ من يسألني فأعطيه؟ من يستغفرني فأغفر له )) البخاري و مسلم
Imetoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: (Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Huteremka (kwa namna inavyolingana na utukufu Wake) kila siku katika mbingu ya dunia (mbingu ya kwanza) inapobakia thuluthi ya mwisho ya usiku na Husema: Nani ananiomba Nimtakabalie? Nani ana shida Nimtekelezee? Nani ananiomba maghfirah Nimghufurie?)) [Al-Bukhaariy na Muslim]


Nani miongoni mwetu asiyemhitaji Mola wake kumkidhia haja zake na kumuondeshea shida zake? Nani asiyekuwa na madhambi asiyemhitaji Mola wake kumghufuria? Hivyo usiache wakati huu ukakupita khaswa kwa vile mwezi huu Mtukufu ambao kila jambo ulifanyalo lina fadhila na thawabu marudufu.
Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atuwezeshe kudiriki nyakati hizo tatu na nyingine, tuwe katika ibada katika mwezi huu wa Ramadhaan na miezi yote mingineyo na Atujaalie kheri na Baraka nyingi, Atukidhie haja zetu, Atuondoshee shida zetu na Atughufurie madhambi yetu yote. Aamiyn.

NASIHA 40 ZA RAMADHAN

Nasiha 40 Za Ramadhaan – Zitekeleze Ufaidike na Mwezi Mtukufu
  
1-Anza kwa kuzingatia mwezi huu mtukufu uwe wa kujihesabu, kutenda amali nyingi na kujirekebisha hali yako na uhusiano wako na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) uwe bora zaidi:  
2- Kumbuka kwamba huu mwezi ni mgeni ambaye amekutembelea kisha ataondoka, hivyo mpokee mgeni wako na mkirimu kwa mazuri yote anayostahiki.  
3-Tahadhari na kutokufunga bila ya sababu au udhuru wowote, kwani kufanya hivyo, Swawm yako haitolipika hata ukifunga mwaka mzima. 
4-Swali kwa wakati wake, usiache Swalah ikakupita. Na jua kuwa ukiwa huswali Ramadhaan huna Swawm kwa mujibu wa fatw za Maulamaa wengi.
5-Soma sana Qur-aan kadiri uwezavyo kwani ni mwezi ulioteremshwa Qur-aan. Kamilisha msahafu mzima japo mara moja, ukishindwa basi hata nusu yake, robo yake. 
6-Zidisha ibada za Sunnah, kama Sunnah zilizo Muakkadah (zilizosisitizwa) na zile Ghayri Muakkadah (zisizosisitizwa). Tazama ratiba katika kiungo kifuatacho:
7-Chukua fursa kuomba du'aa sana kila mara nyakati za kukubaliwa du'aa, khaswa ukiwa bado katika Swawm. Tumia wakati wa baina ya adhana na iqaamah kuomba du'aa na haja zako kwani ni wakati wa kukubaliwa du'aa. Vile vile nyakati za thuluthi ya mwisho ya usiku.
8-Iborishe Swalah yako kwa kuiswali ipasavyo na kuzidisha khushuu (unyenyekevu).
9-Usiache kuswali Taarawiyh pamoja na jama‘ah, usiondoke hadi Imaam amalize upate thawabu za Qiyaamul-Layl. 
10-Tahadhari na kufanya israaf ya mali, chakula na neema nyinginezo, kwani israaf ni mbaya na itakuondoshea neema ulizojaaliwa. 
11- Tumia wakati wako vizuri na zingatia kwamba umri wako unazidi kupunguka. 
12-Mwezi huu ni wa ibada na sio kula, kulala na kufanya ya upuuzi.

13-Zoesha ulimi wako uwe umerutubika kwa kumtaja Mola wako, usiwe miongoni mwa wasiomkumbuka Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) ila kidogo tu. 
14-Chukua fursa kufanya da‘awah. Amrisha mema na kataza maovu, kwani yule unayemuongoza atakapotekeleza mema, utazibeba nawe thawabu zake pia. Tuma ujumbe wa dini kwa wenzako. Chapisha idadi nyingi ya makala zenye mafunzo ya dini, chapisha du'aa ugawe misikitini, vyuoni, majumbani. Unaweza kupata makala na du'aa mbali mbali katika www.alhidaya.com.  Pia kama una uwezo zaidi rekodi mawaidha yaliyomo ndani ya tovuti na wagawie wenzako upate ujira zaidi. Gawa bure na usiuze, kwani si ya kuuzwa. 
15-Fanya kila aina ya wema uwezavyo, patanisha waliokhasimiana, msaidie mwenye haja na muokoe mwenye shida. 
16-Wakumbuke wazazi, ndugu, jamaa na marafiki katika du'aa zako kwani kuwaombea wao bila ya wao kujua Malaika hukuombea na wewe vile vile.
17-Wasiliana na ndugu, jamaa kwani ni jambo lililosisitizwa sana na lenye kukuongeza umri, kheri na baraka nyingi. Walio mbali na wewe wasiliana nao kwa simu.
18-Unapohisi njaa, wafikirie masikini wasio na uwezo wa kula, na utambue kuwa uko katika neema ya Mola wako.
  19-Muombe msamaha uliyemdhulumu kabla hajalipwa mema yako.
 20-Mfuturishe aliyefunga upate thawabu zake juu ya thawabu zako. 
21-Omba maghfirah na msamaha kwa Mola wako, kwani tambua kwamba Yeye ni Mwingi wa Msamaha na Mwingi wa Rahma.
22-Ikiwa umetenda maasi kisha Akakusitiri Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala), tambua kuwa hiyo ni onyo utubie na weka azma kutokurudia tena. 
23- elimu ya dini yako kwa kujifunza tafsiyr ya Qur-aan, Hadiyth, Fiqhi n.k. upate kuongeza taqwa. 
24-Sikiiza mawaidha japo moja kwa siku kwani kusikiliza kunaleta taathira kubwa ya kuongeza Iymaan na Ucha Mungu.
25-Jiepushe na marafiki waovu na vikao vyao na ungamana na marafiki wema na vikao vya kheri.
26-Usipoteze muda wako kutazama televisheni vipindi visivyokupa faida na dini yako, bali tumia wakati wako kwa yatakayokuongezea elimu na ucha Mungu.

27-Usiharibu Swawm yako kwa kunena ya upuuzi, au Ghiybah (kusengenya), au kubishana au kupandisha sauti. Jizuie unapokuwa na hamaki.
28-Fika msikitini mapema zaidi, kwani hivyo ni dalili ya hamu na mapenzi ya ibada na kuwa karibu na Mola wako.
29-Waamrishe na kuwafunza mema ya dini yao walio katika majukumu yako; mke, mume, watoto, ndugu, jamaa n.k. kwani wako karibu yako zaidi na kukutii. 
30-Usijaze tumbo sana katika suhuur (daku) kwani itakufanya uwe mvivu na ushindwe kukaa macho nyakati za asubuhi na mchana na ushindwe kufanya ibada vizuri na kusoma sana Qur-aan.   
31-Usijaze tumbo sana katika iftwaar (kufuturu) kwani itakushinda kusimama Qiyaamul-Layl au kuzingatia Aayah za Qur-aan zinaposomwa na Imaam.
32-Punguza kwenda madukani/sokoni khaswa kumi la mwisho kwani utakosa kheri na thawabu nyingi zilizomo katika masiku hayo ya thamani kubwa.
33-Tilia hima kubwa kuswali Qiyaamul-Layl kumi la mwisho upate Laylatul-Qadr, usiku ambao ibada yake ni bora kuliko miezi elfu.
34-Jitahidi ufanye I'tikaaf msikitini katika kumi la mwisho japo siku chache, upate fadhila zake na uchume mema mengi pamoja na kupata Laylatul-Qadr.  
35-Tambua kwamba siku ya 'Iyd ni siku ya kumshukuru Mola wako na sio siku ya kutenda yale uliyojizuia ya maovu katika Ramadhaan.
36-Siku ya 'Iyd , wafanyie wema wazazi, watembelee ndugu, jamaa na marafiki kuboresha uhusiano wako nao 
37-Usiache kutoa Zakatul-Fitwr - wakumbuke maskini, yatima na wanaohitaji na wasaidie na kuwagawia chochote wabakie katika furaha.
38-Tamka Takbiyrah siku ya 'Iyd kwa sauti unapokwenda msikitini ili kuwakumbusha wengine wanaokwenda au kufuatana nawe ili nawe waweze kupiga Takbiyrah hizo.
39-Weka azma baada ya Ramadhaan kujiendeleza katika hali ya ibada uliyokuwa nayo katika Ramadhaan, ukifanya hivyo itakuwa ni dalili ya kukubaliwa Swawm yako 
 40- Funga Sita Shawwaal upate thawabu za Swawm ya mwaka mzima.

Thursday, July 28, 2011

KARIBU MWEZI MTUKUFU WA RAMADHAN

KARIBU MWEZI MTUKUFU WA RAMADHAAN

Bismillah Ar-Rahmaan-Ar-Rahiim

* يا أيها الذين آمنوا كتب عليكم الصيام كما كتب على الذين من قبلكم لعلكم تتقون*

"Enyi Mlio amini! Mmelazimishwa kufunga saumu kama walivyolazimishwa wa kabla yenu ili mptate kumcha Mungu. "

   
184. (Mfunge) siku maalumu za kuhisabika. Na atakaye kuwa miongoni mwenu mgonjwa au yumo safarini basi atimize hisabu katika siku nyengine. Na wale wasio weza, watoe fidiya kwa kumlisha masikini. Na atakaye fanya wema kwa kujitolea, basi ni bora kwake. Na mkifunga ni bora kwenu, kama mnajua.


 
185. Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa humo Qur'ani kuwa ni uwongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za uwongofu na upambanuzi. Basi ataye kuwa mjini katika mwezi huu naafunge. Na mwenye kuwa mgonjwa au safarini, basi atimize hisabu katika siku nyengine. Mwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito, na mtimize hiyo hisabu, na mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa kuwa amekuongoeni ili mpate kushukuru.